Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana (Jumatatu) katika kikao na wabunge wa Iran na kutoa maelezo kuhusu hali halisi ilivyo hivi sasa katika siasa za nje za Iran hususan upande wa mazungumzo ya Vienna na matukio ya Ukraine.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa ufafanuzi kuhusu mazungumzo ya nyuklia ya Vienna na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inakaribisha juhudi zote za kuharakisha kufikiwa makubaliano mazuri na imara na wakati huo huo lakini, iko imara katika kulinda na kuchunga mistari yake myekundu hasa suala la kupewa dhamana za kutekelezwa vipengee vya makubaliano hayo na kulindwa kikamilifu manufaa ya kitaifa ya Iran.
Awamu ya nane ya mazungumzo ya Vienna kwa ajili ya kuiondolea Iran vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa na Marekani, iliendelea tarehe 8 mwezi ulioisha wa Februari, yaani baada ya siku 11 za mapumziko ambapo timu za mazungumzo hayo zilikuwa zimerejea katika nchi zao kwa ajili ya mashauriano zaidi.
Kabla ya hapo pia, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh alikuwa amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inachukua maamuzi kwa mujibu wa nyenendo za Marekani na si kwa mujibu wa jumbe zisizo wazi za nchi hiyo katika mazungumzo ya Vienna.
Amesema, nchi wanachama katika mapatano ya JCPOA zinajua wazi kwamba Marekani imejitoa kwenye mapatano hayo na inataka kurejea; wajibu ambao inapasa kuukubali wazi mbele ya Iran na mbele ya nchi za kundi la 4+1.
342/